Monday, December 16, 2013

Historia ya Bumbuli...

Bumbuli ni moja ya vijiji vya zamani sana katika nchi ya Tanzania. Kiongozi wa jadi aliyekuwa anaongoza Bumbuli kabla ya uhuru alikuwa anaitwa Zumbe Daudi Sozi Kibanga Moja ya sifa za kiongozi huyu ilikuwa kuleta mvua, tofauti na viongozi wa makabila mengine Zumbe Daudi Sozi Kibanga alikuwa haleti mvua kwa njia ya uganga au uchawi la hasha. Zumbe Daudi alikuwa na kipawa cha kuomba (sala) kwa mwenyezi Mungu na wananchi wakapata mvua. Mahali alipokuwa anakaa Zumbe Daudi palikuwa panaitwa Kitaa. Kabla ya kuja Wamisionari wa Kwanza wa Kijerumani katika eneo hili kijiji kilikuwa kimoja kinachoitwa Kungutana. Baada ya kuja Wamisionari wa Kwanza wa Kijerumani walivutiwa sana na eneo hili ndipo walipowashawishi wananchi kuhamia maeneo mengine ili waweze kujenga Kanisa na shule katika eneo hilo la Kungutana. Wananchi wa eneo hilo walihama eneo hilo na wengi walihamia kijiji kinachoitwa Bumbuli Kaya, mita 200 tu kutoka Kungutana na wengine walihamia eneo jipya linalojulikana kama Bumbuli Mission. Wamisionari wa Kijerumani walijenga shule mbili na Kanisa. Shule ya Maduda ambayo ilikuwa middle school kwa wakati huo. Na nyingine inaitwa Shule ya Msingi Bumbuli na Kanisa la Kilutheri lipo mpaka leo.
Wajerumani hawa waliendelea na kujenga hospitali kubwa sana katika eneo hilo na kwa sababu wamisionari hawa wa Kijerumani walikuwa Walutheri basi baada ya uhuru hospitali hiyo haikutaifishwa na serikali kama uliokuwa mfumo wa wakati huo wa kutaifisha mashirika binafsi bali ilipewa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ili liendelee kuiendesha. Hospitali hiyo inaitwa Bumbuli hospitali.

No comments:

Post a Comment