Ni kwa muda mrefu
sasa nasikia, kuona na kusoma kwenye vyombo vya habari juu ya miaka
kadhaa ya uhuru. Tarehe 9 Desemba mwaka huu, wapo wanaosema ni
maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru wa Tanzania, wengine wanasema miaka 52
ya uhuru wa Tanzania Bara, na wapo pia wanaosema miaka 52 ya uhuru wa
Tanganyika. Swali la kwanza kunijia akilini, kati ya hao wote ni wapi
walio sahihi?
Nchi ya Tanganyika
ilipata uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 1961 na Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere akaapishwa kuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi huru hiyo. Tarehe
kama hiyo ya mwezi Desemba mwaka 1962 Tanganyika ikawa jamhuri na hivyo
kumfanya Mwalimu Nyerere kuapishwa kuwa rais wa kwanza wa Tanganyika.
Tarehe 26 Aprili
mwaka 1964, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tanganyika ikaungana na
Zanzibar kutengeneza nchi mpya inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Jamhuri hiyo ya Muungano inadumu hadi sasa. Siku hiyo Mwalimu
Nyerere aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Siku hiyo pia nchi ya Tanganyika ilikufa rasmi.
Kwa hiyo tukisema
kundi la kwanza la watu wanaosema tunasherehekea miaka 52 ya uhuru wa
Tanzania ndio liko sahihi, tutakuwa kwanza tunajidanganya wenyewe,
tunawadanganya wanetu, wajukuu zetu na ulimwengu mzima kwa kuwa nchi ya
Tanzania inafikisha miaka 52 tarehe 26 Aprili mwaka 2016 kwa kuwa
imezaliwa tarehe hiyo mwaka 1964. Lakini pia tutakuwa hatuwatendei haki
Wazanzibari kwa kuwachanganya kwenye jambo lisilowahusu.

No comments:
Post a Comment